





























Hadeeth Cards
Da'wa cards that highlight great meanings from the noble prophetic hadiths in a simple style and attractive display that helps the Muslim to have a deeper understanding of his religion in an easy way
All
Imepokewa Kutoka kwa bin Abbas -Radhi za Allah ziwe juu yao yeye na baba yake- Kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- katika yale anayoyapokea kutoka kwa Mola wake Mtukufu amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu amepanga mema na mabaya, kisha akalibainisha hilo, atakayekusudia kufanya jema akawa hakulifanya Mwenyezi Mungu humuandikia jema moja kamili, ikiwa atapania na akalifanya Mwenyezi Mungu humuandikia kwake mema kumi mpaka ziada ya mia saba, mpaka kufikia nyongeza ya juu zaidi, na atakayekusudia jambo baya na akawa hakulifanya Mwenyezi Mungu humuandikia kwake jema moja kamili, ikiwa atapania na akalifanya Mwenyezi Mungu humuandikia kwake dhambi moja."
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa Mwenyezi Mungu amepanga mema na maovu, kisha akawabainishia Malaika wawili ni namna gani watayaandika: Atakayetaka na akakusudia na akaazimia kufanya jema basi litaandikwa kwake jema moja, hata kama hatolifanya, na ikiwa atalifanya basi hulipwa mara dufu kwa mara kumi mfano wake, mpaka ziada ya mia saba, mpaka ziada nyingi zaidi, na ziada huendana na yale yaliyoko moyoni kwanzia Ikhlaswi (kutakasa nia) na kuwanufaisha wengine, n.k. Na atakayetaka na akakusudia na akaazimia kufanya uovu kisha akauacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huanidikiwa jema moja, na ikiwa atauacha kwa sababu ya kukosa muda wa kuufanya na akiwa hajafanya sababu za kuuendea, hatoandikiwa chochote, na akiuacha kwa kushindwa huandikwa nia yake pekee, na ikiwa ataufanya litaandikwa kwa ovu moja.
Kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Hakika Mwenyezi Mungu hatazami sura zenu na mali zenu, lakini anatazama katika nyoyo zenu na matendo yenu."
Imepokelewa Imamu MuslimAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hatazami sura za waja na miili yao, je ni nzuri au mbaya? Je ni mikubwa au midogo? Ina afya au maradhi? Na wala hatazami katika mali zao, je ni nyingi au kidogo? Mwenyezi Mungu -Aliyetakasika na kutukuka hawaadhibu waja wake wala hawahesabu kwa mambo haya na kutofautiana kwao, lakini anatazama katika nyoyo zao na yale yaliyomo ndani miongoni mwa uchamungu na yakini, na ukweli na ikhlaswi, au ni lengo la kujionyesha au kutaka kusikika, na anatazama katika matendo yao upande wa usahihi wake au kuharibika kwake; Hapo atatoa thawabu na malipo kwa hayo.
Imepokewa Kutoka kwa Omar bin Khattwab -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Siku moja tukiwa tumekaa kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- ghafla akatokea mtu mwenye nguo nyeupe mno, mwenye nywele nyeusi mno, haonekani kuwa na athari yoyote ya safari, na hakuna yeyote amjuaye miongoni mwetu, akaja mpaka akakaa kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akakunja magoti yake kwa kuyaunganisha na magoti yake mtume (Mithili ya tahiyatu) Na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake, na akasema: Ewe Muhammadi, nieleze kuhusu Uislamu, akasema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Uislamu ni ushuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na usimamishe sala, na utoe zake, na ufunge Ramadhani, na uhiji katika nyumba tukufu ikiwa utapata uwezo wa kuifikia" Akasema: Sadakta! (Umesema kweli), Anasema: Tukamshangaa: Anamuuliza na anamsadikisha! Akasema: Nieleze kuhusu imani. Akasema: "Nikuwa, umuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na vitabu vyake, na Mitume wake, na siku ya mwisho, na uamini Kadari kheri yake na shari yake" Akasema: Sadakta! (Umesema kweli), akasema: Nieleza kuhusu Ihisani, akasema: "Ni umuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona, na ikiwa wewe humuoni basi yeye anakuona" Akasema: Nieleze kuhusu Kiyama, akasema: "Muulizwaji si mjuzi sana kama muulizaji" Akasema: Hebu nieleze kuhusu alama zake, akasema: "Ni mjakazi kuzaa bosi wake, na ukiwaona watembea peku, watembea uchi, tena masikini wachunga mbuzi, wakishindana kujenga majengo marefu." (Omar) Akasema: Kisha akaondoka, nikakaa muda mrefu kidogo, kisha Mtume akasema kuniambia: "Ewe Omari, hivi unamjua ni nani muulizaji?" Nikasema: Allah na Mtume wake ndio wajuzi zaidi, akasema: "Huyo ni Jibrili alikuja kukufundisheni dini yenu."
Imepokelewa Imamu MuslimAnaeleza Omari bin Khattwab -Radhi za Allah ziwe juu yake- kuwa Jibrili -Amani iwe juu yake- alijitokeza kwa Masahaba -Radhi za Allah ziwe juu yao- kwa sura ya mtu asiyejulikana, na miongoni mwa sifa zake nikuwa, nguo zake ni nyeupe mno, na nywele zake ni nyeusi mno, haonekani kuwa na athari za safari ikiwemo kuonyesha uchovu, vumbi, na nywele kutimka, na nguo kuchafuka, na hakuna yeyote amjuaye katika wote waliopo, nao wakiwa wamekaa kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akakaa mbele ya Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- mkao wa mwanafunzi, akamuuliza kuhusu Uislamu, akamjibu kwa nguzo hizi ambazo zimeambatana na kukiri shahada mbili, na kudumu na sala tano, na kutimiza zaka kwa wastahiki wake, na kufunga mwezi wa Ramadhani, na kutekeleza faradhi ya Hija kwa mwenye uwezo. Muulizaji akasema: Sadakta!, Masahaba wakashangaa kwa swali lake la kuonyesha kuwa hajui kitu kwa muonekano wake, kisha anamsadikisha!. Kisha akamuuliza kuhusu imani, akamjibu kwa nguzo hizi sita zilizokusanya kuamini uwepo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa zake, na kumpwekesha kwa vitendo vyake kama kuumba, na kumpwekesha kwa ibada, nakuwa Malaika aliowaumba Allah kwa nuru ni waja waliotukuzwa hawamuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu, na amri yake ndio wanayoifanyia kazi, na kuamini vitabu vilivyoteremshwa kwa Mitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama Qur'ani na Taurati na Injili na vinginevyo, na kuwaamini Mitume wenye kumfikishia Mwenyezi Mungu dini yake, miongoni mwao ni Nuhu na Ibrahim, na Mussa, na Issa, na wa mwisho wao ni Muhammadi -Rehema na amani ziwe juu yao wote- na wengineo katika Manabii na Mitume, na kuamini siku ya mwisho, na yanaingia hapa maisha baada ya kifo ikiwemo kaburi na maisha ya barzakh (Akhera), na kuamini kuwa Mwenyezi Mungu amekadiria mambo kulingana na ujuzi wake uliotangulia na hekima zake zikapelekea hivyo, na kuyaandika kwake, na matashi yake kwa mambo hayo, na kutokea kwake kwa namna aliyoikadiria Mwenyezi Mungu, na kuviumba kwake. Kisha akamuuliza kuhusu Ihisani, akamueleza kuwa Ihisani ni amuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba anamuona, ikiwa hatoweza kufikia daraja hili basi amuabudu Allah kana kwamba Allah anamshuhudia, daraja bora zaidi kushuhudiwa, na ndio ya juu zaidi, na ya pili ni daraja ya kuchunga (Kuleta hisia kua unamuona mbele yako). Kisha akamuuliza Kiyama ni lini? Akabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa elimu ya Kiyama ni katika elimu alizobaki nazo Mwenyezi Mungu ujuzi wake, hawezi kuijua yeyote katika viumbe, si muulizaji wala muulizwaji. Kisha akamuuliza kuhusu alama za Kiyama? Akabainisha kuwa miongoni mwa alama zake ni kukithiri kwa wajakazi (Masuria) na watoto wao, au ni wingi wa watoto kutowatii mama zao, kiasi cha kuishi nao kama watumwa wao, nakuwa wachunga mbuzi na masikini watakunjuliwa dunia katika zama za mwisho, na watafaharishana katika kuremba majengo na kuyarefusha. Kisha akaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa muulizaji ni Jibril alikuja kuwafundisha Masahaba dini tukufu.
Kutoka kwa Aisha -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakayezua katika dini yetu hii, yale yasiyokuwemo, basi yatarejeshwa" Kaipokea Bukhari na Muslim. Na kutoka kwa Muslim: "Atakayefanya amali yoyote isiyokuwa na amri yetu, basi itarejeshwa".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa atakayetunga au kubuni jambo katika dini au akafanya amali yoyote ambayo haikuelekezwa na dalili yoyote kutoka katika Qur'ani na Sunna, basi jambo hilo litarejeshwa kwa mfanyaji wake na halitokubaliwa mbele ya Allah.
Imepokewa kutoka kwa Abuu Dharri -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-: Kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-katika yale aliyoyapokea kutoka kwa Mola wake Mtukufu hakika Yeye amesema: "Enyi waja wangu hakika Mimi nimeharamisha dhulma juu ya Nafsi yangu na nikaifanya kuwa ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane, enyi waja wangu nyote ni wapotevu isipokuwa yule niliye muongoza, basi niombeni uongofu nami nitakuongozeni, enyi waja wangu nyote ni wenye njaa isipokuwa yule niliye mlisha, basi niombeni chakula nami nitakulisheni, enyi waja wangu nyote mpo uchi isipokuwa yule niliye mvisha, basi niombeni kuvaa nami nitakuvisheni, enyi waja wangu hakika nyinyi mnakosea usiku na mchana na mimi ninasamehe madhambi yote, basi niombeni msamaha nami nitakusameheni, enyi waja wangu hamtafikia kufanya madhara ili mnidhuru wala hamtafanya mambo yenye manufaa ili mninufaishe, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wakijikusanya wote wakawa na ucha Mungu wa mtu mmoja hilo lisinge niongezea chochote katika Ufalme wangu chochote, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wakijikusanya wote wakafanya uovu wa mtu mmoja hilo lisinge punguza chochote katika Ufalme wangu, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wangejikusanya katika uwanja mmoja wakaniomba nikampa kila mtu alicho kiomba hilo lisinge punguza chochote katika Ufalame wangu isipokuwa ni kama sindano inavyo punguza maji pindi inapo ingizwa baharini, enyi waja wangu si vinginevyo bali hakika matendo yenu yote nina wahifadhieni kisha nitawapa malipo yenu, mwenye kupata kheri amshukuru Mwenyezi Mungu, na atakayepata kinyume na hayo basi asimlaumu yeyote isipokuwa nafsi yake."
Imepokelewa Imamu MuslimAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka amesema kuwa amejiharamishia dhulma juu ya Nafsi yake, na akaifanya dhulma kuwa haramu baina ya waja wake, hivyo mtu asimdhulumu yeyote, Nakuwa viumbe wote wamepotea katika njia ya haki isipokuwa kwa uongofu wa Mwenyezi Mungu na taufiki yake, na atakayemuomba Mwenyezi Mungu uongofu basi atamuafikisha na atamuongoza, Nakuwa viumbe wote ni mafukara kwa Mwenyezi Mungu, wote ni wahitaji kwake katika haja zao zote, na atakayemuomba Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamtimizia haja zake na atamtosheleza, Nakuwa wao hutenda dhambi usiku na mchana, na Mwenyezi Mungu Mtukufu husitiri na husamehe pale mja anapomuomba msamaha, Nakuwa wao hawawezi kumdhuru Mwenyezi Mungu au kumnufaisha kwa chochote, Nakuwa wao lau kama wangelikuwa katika uchamungu wa moyo wa mtu mmoja, uchamungu wao usingeongeza chochote katika Ufalme wa Mwenyezi Mungu, Na lau kama wangelikuwa katika uovu wa moyo wa mtu mmoja, uovu wao usingepunguza chochote katika Ufalme wake; kwa sababu wao ni madhaifu na mafakiri na ni wahitaji kwake kwa kila hali na kwa nyakati zote na mahala popote, na yeye ni mkwasi na utakasifu ni wake. Na lau kama wangelisimama mahala pamoja binadamu wao na majini wao, wa mwanzo wao na wa mwisho wao, wakimuomba Mwenyezi Mungu, akampa kila mmoja miongoni mwao ombi lake, hilo lisingepunguza chochote katika vile vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa ni kama mfano wa sindano inapoingizwa Baharini kisha ikatolewa, Bahari kamwe haipungukiwi na kitu, na hii ni kwa sababu ya ukamilifu wa utajiri wake Mtukufu. Nakuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anayahifadhi matendo ya waja na kisha anawatunzia, kisha anawatimizia malipo siku ya Kiyama, atakayekuta malipo ya matendo yake yakiwa ni kheri basi na amshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuafikisha kwake katika kumtii, na atakayekuta malipo ya matendo yake ni kinyume na hivyo basi asilaumu ila nafsi yake yenye kuamrisha maovu iliyompelekea katika hasara.
Imepokewa kutoka kwa Bin Abbas -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na baba yake- amesema: Siku moja nilikuwa nyuma ya Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akasema: "Ewe kijana, hakika mimi ninakufundisha maneno, muhifadhi Mwenyezi Mungu naye atakuhifadhi, muhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta uendako, utakapoomba basi muombe Mwenyezi Mungu, na utakapotaka msaada basi taka msaada kwa Mwenyezi Mungu, na tambua kuwa umma mzima lau wangekusanyika ili wakunufaishe kwa chochote, basi wasingelikunufaisha isipokuwa kwa kitu alicho kuandikia Mwenyezi Mungu kuwa chako, na lau kama wangelikusanyika ili wakudhuru kwa chochote, basi wasingeweza kukudhuru isipokuwa kwa kitu alichokiandika Mwenyezi Mungu dhidi yako, kalamu zimenyanyuliwa na kurasa zimekauka".
Imepokelewa Imamu TirmidhiyAnaeleza bin Abbas -Radhi za Allah ziwe juu yake- kuwa yeye alipokuwa kijana mdogo alikuwa kapanda pamoja na Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akasema kumwambia -Amani iwe juu yake-: Hakika mimi ninakufundisha vitu na mambo ambayo Mwenyezi Mungu atakunufaisha kwayo: Muhifadhi Mwenyezi Mungu kwa kuhifadhi maamrisho yake na kuepuka makatazo yake, kiasi kwamba akukute katika utiifu na yale yenye kukuweka karibu naye, na asikukute katika maasi na madhambi, ikiwa utafanya hivyo basi malipo yako yatakuwa ni Mwenyezi Mungu kukuhifadhi kutokana na kero za Dunia na Akhera, na atakunusuru katika mambo yako magumu mahala popote utakapoelekea. Na ukitaka kuomba jambo, basi usimuombe ila Mwenyezi Mungu kwani Yeye pekee ndiye mwenye kuwajibu waombaji. Na ukitaka msaada basi usiutake ila kwa Mwenyezi Mungu. Na uwe na yakini kuwa hutopata manufaa yoyote hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukunufaisha, isipokuwa kwa kile alichokiandika Mwenyezi Mungu kwako, na wala hutopata madhara hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukudhuru, isipokuwa kwa lile alilolikadiria Mwenyezi Mungu juu yako. Na kuwa jambo hili kashaliandika Mwenyezi Mungu Mtukufu na akalikadiria kulingana na namna hekima na elimu yake zilivyopelekea, na hakuna kubadilishwa yale aliyoyaandika Mwenyezi Mungu.
Imepokewa Kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- yakwamba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Umma wangu wote wataingia peponi isipokuwa atakaye kataa" Wakasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na ni nani atakaye kataa? Akasema: "Atakaye nitii ataingia peponi, na atakaye niasi atakuwa amekataa".
Imepokelewa na Al-BukhaariyAnaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakwamba umma wake wote wataingia peponi isipokuwa atakaye kataa!. Masahaba -Radhi za Allah ziwe juu yao- wakasema: Ni nani atakaye kataa ewe Mjumbe wa Allah?! Akawajibu -Rehema na amani ziwe juu yake-: Kuwa atakayejisalimisha na akafuata na akamtii Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- ataingia peponi, na ama atakaye asi na akawa hakujisalimisha katika sheria atakuwa kakataa mwenyewe kuingia peponi kwa sababu ya matendo yake mabaya.
Kutoka kwa bin Omari -Radhi za Allah ziwe juu yake yeye na baba yake- Amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakaye jifananisha na watu fulani basi na yeye ni miongoni mwao".
Imepokelewa na Abu Daud na AhmadAnaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa atakaye jifananisha na watu fulani katika makafiri au waovu au wema -na hii ni pale atakapofanya jambo katika mambo yao mahususi, kama itikadi au ibada au tamaduni basi naye ni miongoni mwao-; kwa sababu kujifananisha nao katika muonekano kunapelekea kujifananisha nao kiundani, na hakuna shaka kuwa kujifananisha na watu fulani kunasababishwa na kupendezwa nao, na huenda kukapelekea kuwapenda na kuwatukuza na kuwategemea, na hili huenda likampelekea mtu hata kujifananisha kiundani na katika ibada -Tunamuomba Allah atukinge na hilo-.
Imepokewa kutoka kwa Abdullahi Bin Masoud -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: Nilimuuliza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: Ni dhambi ipi kubwa zaidi mbele ya Allah? Akasema: "Ni wewe kumuwekea Mwenyezi Mungu mshirika, na hali yeye ndiye aliyekuumba" Nikasema: Hakika hilo ni jambo kubwa, nikasema: Kisha ipi? Akasema: "Na kumuua mwanao; ukiogopea atakula pamoja nawe" Nikasema: Kisha ipi? Akasema: "Ni wewe kumzini mke wa jirani yako".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAliulizwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuhusu dhambi kubwa akasema: Kubwa zaidi ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, nako ni kumuwekea Mwenyezi Mungu mfano katika uungu wake au uumbaji wake au majina yake na sifa zake, na dhambi hili halisamehe Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa toba, na akifa mfanyaji wake huyo atakaa milele motoni. Kisha ni mtu kumuua mwanaye kwa kuchelea kula naye, na kuua nafsi ni haramu, lakini dhambi linakuwa kubwa pale anapokuwa muuliwaji ni ndugu wa damu wa muuaji, na dhambi lake linakuwa kubwa pia pale linapokuwa lengo la muuaji ni kuchelea kushirikiana pamoja na muuliwaji katika riziki ya Mwenyezi Mungu. Kisha ni mtu kumzini mke wa jirani yake kwa kujaribu kumhadaa mke wa jirani yake mpaka akafikia kuzini naye, naye akamkubalia, Na zinaa ni haramu lakini dhambi lake linakuwa kubwa anapokuwa mziniwa ni mke wa jirani ambaye sheria imeusia kumtendea wema na kuishi naye vizuri.